Ni mara chache sana kuona mwanamke anatoka kwenda katika shughuli yoyote bila kubeba mkoba. Iwe mkoba mdogo, wa wastani au mkubwa, haijalishi ukubwa ila ni lazima atoke na mkoba. Leo tunaangalia ni vitu gani ambavyo vinawekwa kwenye mikoba hiyo.
Kwa kawaida mwanamke hubeba mkoba wa wastani ambao ndani yake huwa na kioo kidogo, kanga, vipodozi,kiasi kidogo cha pesa, simu na vitu vingine ambavyo mwanamke atavihitaji kulingana na sababu ya mtoko wake.
Mmoja wa maofisa habari wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Violet Mwangalaba anasema hawezi kwenda sehemu yoyote bila kubeba mkoba kwa sababu huwa na vitu vyote ambavyo huvihitaji kwa siku nzima.
“Lazima nibebe vitambulisho vyangu, mafuta ya mdomoni, manukato madogo, simu, kanga na chaja kwa ajili ya simu yangu,” alisema.
Kila mwanamke atakupa maelezo ambayo yanafanana juu ya mikoba na nini kimo ndani ya mkoba hiyo. Anachobadilisha mwanamke ni ukubwa wa mkoba kulingana na mahali anapokwenda au tukio analokwenda kuhudhuria.Anaendelea kusema kuwa hata kama anaenda kwenye sherehe mbalimbali nyakati za usiku, lazima abebe pochi ndogo itakayokuwa na manukato na mtandio mdogo.
Mikoba inayobebwa kwenda kazini ni tofauti na ile inayobebwa kwenda kwenye sherehe au kuwapeleka watoto kliniki. Tofauti kubwa ipo kwenye ukubwa na vilivyomo ndani.
Mikoba ya kazini huwa na ukubwa wa wastani na huwa na vitu muhimu kwa ajili ya siku nzima ambayo mwanamke anakua kazini, tofauti na mikoba kwa ajili ya kliniki ambapo huwa mikubwa kwani hubeba vifaa kwa ajili ya mama na mtoto.
Kwa ajili ya sherehe, mara nyingi wanawake hubeba mikoba midogo ijulikanayo kama pochi. Huu huwa na uwezo wa kubeba vitu vichache zaidi kama rangi za midomoni (lipstiki), simu na mafuta ya mikono.
Hiyo ndio mikoba ya wanawake. Ila kwa ushauri tu, ni vema vitu vyote vinavyowekwa kwenye mkoba viwe katika mpangilio mzuri ili iwe rahisi kutoa kitu bila kumwaga vitu vyote katika mkoba ili kupata kitu kimoja.
No comments:
Post a Comment